Ukiwa na Tabia Hizi 7, Lazima Mwanaume Akukimbie Tu Hata Kama Una Uzuri Kiasi Gani
1. CHOKOCHOKO
Wanaume wengi huwa hawapendi chokochoko. Hawapendi mwanamke ambaye yeye kila wakati ni kuanzisha chokochoko ambazo zinazalisha ugomvi. Wanaume wengi hawapendi mabishano. Hawapendi ugomvi hivyo mwanamke anapokuwa hodari wa kuleta chokochoko, huepukwa.
Ni vyema basi mwanamke akachunga kauli. Akawa si mtu wa kuchimbachimba vitu ambavyo havina kichwa wala miguu. Asiwe na kisirani. Kinywa chake kitawaliwe na maneno matamu, yatakayomtia moyo mpenzi wake, yatakayomfariji na yatakayomfanya apende kuzungumza naye.
2. KUTORIDHIKA
Wanaume wengi wanachukia kuwa na wanawake wasioridhika. Baadhi ya wanawake hata uwape nini huwa hawaridhiki. Wanawasumbua wapenzi wao kwamba hawawatimizii mahitaji. Mwanaume anajitoa kumpa zawadi mpenzi wake, haridhiki tu.
Anaanza kuikosoa. Anasema haifanani na yeye, eti si ya hadhi yake. Akipewa fedha anasema hazitoshi. Kila siku ni malalamiko. Hampi nafasi mpenzi wake ya kufurahia uhusiano wao. Anamfanya kila anapokutana naye awaze atapigwa mzinga.
3. KULINGANISHA
Hii nayo ni tabia isiyopendwa na wanaume wengi. Wanaume wanapenda kuishi maisha yao. Wanapenda kuheshimiwa na wapenzi wao. Wanapenda kumsikia mwanamke akisema; ‘hakuna mwanaume mwingine wa kufanana na wewe.’
Mwanaume anapenda kuhakikishiwa kwamba hakuna mwanaume mwingine kama yeye. Yeye ndiye mzuri au bora kuliko wanaume wengine hivyo mwanamke anapoanza kuonesha tabia za kumlimnganisha na mwanaume mwingine linakuwa tatizo kubwa.
4. KUWA TEGEMEZI
Wakati mwingine hata kama huna kitu lakini mwanamke unashauriwa kutojionesha huna kitu. Jioneshe kwamba una kitu hata kama huna. Wanaume wa sasa hawapendi kuwa na mwanamke ambaye kila kitu anategemea kutoka kwa mwanaume.
Hata kama huna kazi lakini ni vyema basi mwanamke akajaribu kufanya biashara ndogondogo ambazo zitampunguzia mwanaume wake makali ya kuombwa fedha kila wakati. Wanaume wanapenda kuwapa wapenzi wao fedha lakini inapozidi kipimo inageuka kuwa kero.
5. KUTOKUA MUELEWA
Mwanaume anapenda mwanamke muelewa. Hapendi mwanamke mbishi. Anatamani kuwa na mwanamke ambaye akimueleza kitu, anajiongeza na kufanya zaidi ya pale mwanaume alipofikiria. Mwanaume anapenda mwanamke atakayeanzisha wazo la kimaendeleo na kumshirikisha mpenzi wake ili walifanye.
Wanaume wanapenda wanawake wanaowaelewa. Kama mwanamke anakuwa si wa kumuelewa mpenzi wake, kumsaidia basi mara nyingi mwanaume humkimbia.
6. KUJITAPA KWA KUWA NACHO
Hakuna mwanaume anayependa kutawaliwa. Wanawake wenye fedha mara nyingi wanakuwa na tabia ya kutaka kuwatawala wanaume. Anataka mwanaume afanye kile ambacho yeye anataka. Fedha zinamvimbisha kichwa na kuona kwamba anaweza kuwa na mamlaka ya kumuamrisha mumewe.
Anatumia fedha zake kama fimbo ya kumchapia mpenzi wake. Ni vigumu sana wanaume kumvumilia mwanamke wa aina hiyo, mara nyingi wanajiepusha naye. Kwa kutumia fedha zake anaweza kupata mwanaume mwingine lakini pia watashindwana katika suala la kumtawala.
7. KUWA BIZE SANA
Wanaume wengi hawapendi mwanamke tegemezi lakini pia wanaume haohao wanachukia mwanamke akiwa bize sana na kazi zake. Mwanaume hapendi kuona mwenzi wake anakuwa bize na kazi au biashara zake kiasi ambacho kitamfanya hata akose muda na mwenzi wake.
Unachotakiwa kufanya hapo mwanamke ni kujigawa. Hakikisha unakuwa bize na kazi lakini si ya kupitiliza maana itamfanya mwanaume akose muda wa kuwa na wewe pale anapokuhitaji, badala yake anaweza kwenda kwa mwanamke mwingine ambaye hayupo bize.

Comments
Post a Comment